Shirika la Habari la Hawza - Mwanadamu, akiwa ni kiumbe mwenye mipaka, anakabiliwa na masuala lukuki ya kimwili na kiroho, na yupo katikati ya matamanio ya haki na batili yatokayo na yeye mwenyewe au kutoka kwa wengine. Katika hali hii anahitaji hifadha imara, na hifadha bora zaidi ni Mwenyezi Mungu. Mwanadamu hana njia nyingine isipokuwa kusonga na kumkimbilia Mwenyezi Mungu. (1)
Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema katika Qur’ani Tukufu:
«فَفِرُّوا إِلَی اللَّهِ»
“Basi kimbilieni kwa Mwenyezi Mungu.” (2)
Sherehe:
Katika maandiko na vitabu mbalimbali (3), maneno haya yamehusishwa na Aflaton ambayo yanaweza kutusaidia katika kuifahamu aya hii ya Qur’ani. Imepokewa kutoka kwake kwamba alisema:
«العالم کرة»Ulimwengu ni wa mviringo.
«والأفلاک قِسیٌّ»
Mbingu ni kama upinde (katika ulimwengu huu).
«والحوادث سِهامٌ»
Matukio ni mishale ya upinde huo.
«و الانسانُ هدفٌ»
Na binadamu ndiye shabaha.
«و الرّامی هو الله تعالی»
Na mtupa mishale ni Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Kisha Aflaton anahoji kwa undani:
«فأینَ المَفَر؟»
“Basi pa kukimbilia ni wapi? Unataka kukimbilia kwa nani?”
Jibu la swali la Aflaton linapatikana katika maneno yale yale ya Qur’ani:
«ففِرُّوا إِلَی اللَّهِ؛
Basi kimbilieni kwa Mwenyezi Mungu.»
Nukta nyeti ya kuzingatia: Ni wapi katika ulimwengu huu tumeona mwindwaji akikimbilia kwa mwindaji wake? Kawaida ya kimaumbile na kiakili ni kwamba mwindwaji humkimbia mwindaji, si kwenda kwake. Lakini hadithi ya Mwenyezi Mungu ni tofauti kabisa. Ndiyo maana Imam Sajjad (a.s.) anamsemesha Mwenyezi Mungu kwa maneno haya:
«یَا مَنْ لامَفَرَّ إِلا إِلَیْهِ، یَا مَنْ لا مَفْزَعَ إِلا إِلَیْهِ، یَا مَنْ لا مَقْصَدَ إِلا إِلَیْهِ، یَا مَنْ لا مَنْجَی مِنْهُ إِلا إِلَیْهِ، یَا مَنْ لا یُرْغَبُ إِلا إِلَیْهِ، یَا مَنْ لا حَوْلَ وَ لا قُوَّةَ إِلا بِهِ، یَا مَنْ لا یُسْتَعَانُ إِلا بِهِ، یَا مَنْ لا یُتَوَکَّلُ إِلا عَلَیْهِ، یَا مَنْ لا یُرْجَی إِلا هُوَ، یَا مَنْ لا یُعْبَدُ إِلا هُوَ.»
“Ewe ambaye hakuna pa kukimbilia isipokuwa Kwake, ewe ambaye hakuna kimbilio isipokuwa Kwake, ewe ambaye hakuna shabaha isipokuwa kwake, ewe ambaye hakuna wokovu kutoka Kwake ila kwa kukimbilia Kwake, ewe ambaye hamu na matarajio yote ni Kwake, ewe ambaye hakuna nguvu wala uwezo ila kwake yeye, ewe ambaye hakuna msaada wowote ila kutoka Kwake, ewe ambaye hakuna wakutegemewa isipokuwa kwake yeye, ewe ambaye hakuna matumaini ila Kwake, ewe ambaye hakuna anayeabudiwa isipokuwa yeye.” (4)
Kwa nini tunapaswa “kumkimbilia” Mwenyezi Mungu?
Imam Swadiq (a.s.) anaweka wazi jambo hili katika hadith mashuhuri, akisema:
«کُلُّ ذِکْرٍ سِوَی اَللَّهِ ظُلْمَةٌ.»
“Kila utajo usiyo kuwa wa kumkumbuka Mwenyezi Mungu ni kiza.” (5)
Kwa hiyo ni jambo la busara kwa mwanadamu kukimbia mbali na iza, mbali na kila kilicho na harufu ya kigeni kwa Mungu, na kimbilio la kweli ni Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Ikiwa mtu hapa duniani hakumkimbilia Mungu, wala hakuepuka na kumtegemea asie kuwa Yeye, basi Siku ya Kiyama atalazimika kuwakimbia wote wasiokuwa Mungu, Kama Qur’ani inavyosema:
«یَوْمَ یَفِرُّ الْمَرْءُ مِنْ أَخِیهِ، وَ أُمِّهِ وَأَبِیهِ، وَصَاحِبَتِهِ وَبَنِیهِ.»
“Siku hiyo mwanadamu atamkimbia ndugu yake, na mama yake na baba yake, na mke wake na watoto wake.” (6)
Rejea:
1. Tafsīr Nūr
2. Sura adh-Dhāriyāt, aya ya 50
3. Ganjīna-ye Akhlāq (Jāmiʿ al-Durar), Juzuu ya 2 / Tawba: Sharh-e Duʿā-ye 31 ya Ṣaḥīfa Sajjadiyya, n.k.
4. Duʿāʾ al-Jawshan al-Kabīr
5. Miṣbāḥ al-Sharīʿa, Juzuu ya 5, uk. 192
6. Sura ʿAbasa, aya 34–36
Imeandaliwa na Kitengo cha Elimu na Utamaduni cha Shirika la Habari la Hawza.
Maoni yako